GLDA

GLDA ni kifupi cha Gitemi Language Development Association (Shirika la Maendeleo ya Lugha ya Gitemi). GLDA ni shirika lisilo la Kiserikali lililosajiliwa kwa mujibu wa sheria kama shirika la Kijamii (CBO). Lilianza kuundwa na jamii ya Batemi mwaka wa 2012 na mwaka wa 2013 kusajiliwa rasmi kama CBO. Shirika hili limeundwa kwa lengo la kuendeleza lugha ya Gitemi. Wana GLDA tunaendeleza lugha ya Gitemi kwa: Kuandika, Kufundisha kusoma na kuandika, Tafsiri ya vitabu mbalimbali ikiwemo Biblia, Tafiti mbalimbali kuhusu lugha na tamaduni za Batemi pamoja na kuelimisha jamii. Makao makuu ya GLDA yapo katika kijiji cha Digodigo, kata ya Digodigo, tarafa ya Sale, mkoani Arusha.

 MAONO YA GLDA NI:

Kuhifadhi lugha ya Gitemi kwa njia ya maandishi katika vitabu.

UTUME WA GLDA NI:

Kuhakikisha kuwa lugha ya Gitemi inaandikwa, kusomwa, na kutumika.

LENGO KUU LA GLDA NI:

Madhumuni ya GLDA ni kuandika lugha ya Gitemi ili kuwasaidia Batemi waweze kusoma na kuandika lugha yao.

MALENGO MAHUSUSI YA GLDA NI:

  1. Kuisaidia jamii ya Batemi kuandika lugha yao
  2. Kutafsiri vitabu mbalimbali pamoja na Biblia kwa lugha ya Gitemi.
  3. Kuandaa na kutoa kamusi ya lugha ya Gitemi
  4. Kutunza lugha ya Gitemi kwa njia ya maandiko
  5. Kufundisha jamii kutumia fasihi na sanaa katika kuhifadhia lugha                                                    

SHUGHULI  ZA GLDA NI:

  1. Kutafsiri maandiko, vitabu, majarida na  Biblia  kwa lugha ya Gitemi
  2. Kufundisha jamii ya Batemi kusoma na kuandika lugha yao
  3. Kuandika na kuchapisha vitabu, makala, majarida nk kwa lugha ya Gitemi
  4. Kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kufundisha jamii juu ya mambo mbalimbali
  5. Kuisaidia jamii kutokomeza mila hatarishi
  6. Kuandaa kamusi ya lugha ya Gitemi

UANACHAMA

Uanachama wa GLDA utakuwa ni wazi kwa mtu yeyote ambaye anakubaliana na madhumuni ya shirika hili. Anayetaka kujiunga atatuma maombi kwa katibu wa shirika na barua ya mwombaji itapelekwa kwa kamati tendaji. Barua ya mwombaji itajadiliwa ikionekana kuwa mwombaji anafaa, ombi lake litapelekwa kwa mkutano mkuu ambao ndio watakaokuwa na uwezo wa kumkubali au kumkataa.

AINA ZA WANACHAMA

Kutakuwa na aina tatu za wanachama wa shirika hili ambao ni;

Wanachama waanzilishi, wanachama wa kawaida, wanachama wa heshima.

                                                      I.  Wanachama waanzilishi ni wale walioanzisha shirika na kuidhinisha katiba hii na  watakuwa ndio wenye shirika.

II. Wanachama wa kawaida ni wale watakaojiunga na shirika baada ya shirika kupanuka. Wanachama hawa watagawanyika mara mbili. Mtu binafsi na taasisi. (i) Mtu binafsi atajiunga na shirika bila kutumwa na taasisi kwa kutuma maombi kwa katibu. (ii) Taasisi itatuma maombi kwa katibu na wakikubaliwa watamtuma mtu wao atakayekuwa anawawakilisha.

 

III. Wanachama wa heshima katika shirika hili ni wanachama watakao jiunga na shirika wakiwa na vyeo katika taasisi zao, k.m Watumishi kutoka taasisi mbalimbali.

 

Kwa wanachama wapya watatakiwa kutoa kiingiliao chao ndani ya Shirika na kiingilio hiki kitapangwa na mkutano mkuu na mwombaji atajulishwa.

Your encouragement is valuable to us

Your stories help make websites like this possible.