Jina la 'Sonjo' Limetoka Wapi

Tangu karne iliyopita, Batemi walikuwa wameitwa kwa jina la ‘Sonjo.’  Watu wanaitwa ‘Wasonjo’ na lugha yao inaitwa ‘Kisonjo.’ Pia eneo wanaloishi linaitwa ‘Sonjoni.’  Badala ya kusema hawa ni ‘Batemi,’ wanazungumza lugha ya ‘Gitemi,’  na nyumbani ni ‘Butemine,’ neno hili la ‘Sonjo’ lipo kila mahali. Je, imetokeaje? Soma stori hii ya kuchekesha:

Wakati wa wakoloni, Batemi walikuwa wakizungusha vijiji vyao na ua wa miiba. Wakati ule, hawakuwana barabara ya kufika vijijini, na safari ya kwenda Arusha ilichukua zaidi ya siku tatu kwa kutembea. Wao waliosafiri walikuwa morani tu, hawa batana.

Wakoloni walikuwa na ofisi kuu mlimani Loliondo, umbali wa kilometa sitini. Lugha ya Kiswahili ilijulikana sehemu za pwani, lakini ndani ya Tanganyika, watu wachache walifahamu kuongea lugha hii.

Basi, siku moja mkoloni akatoka ofisini akielekea Butemini. Lengo lake ilikuwa kufanya upelelezi kwa swali hili, “Ni watu gani wanaoishi eneo hili?” Akakaribia shambani, na kuona wanawake waliolima pamoja. Wakati ule wanawake walitumia kijiti kirefu cha kulimia, yaani mulɔ.

Nao walishtuka pia! Wakaulizana kwamba, ”Je? Huyu ni mtu gani? Mbona haongei lugha yetu? Anasemaje? Mbona nguo zake ni za ajabu ajabu?”

Mwanaume huyu  akawauliza, “Je, nyinyi ni watu gani? Mnaongea lugha gani?" Wale wanawake hawakumwelewa, “Mbona anauliza kwamba tunapanda nini shambani?" Walikuwa wakipanda fiwi, kwa lugha ya Gitemi, ni ‘sonjo.’

“Nyinyi  ni watu gani?”

Sonjo.”

“Nyinyi ndiyo ni Wasonjo??”

Eeh, sonjo.

Basi! Huyu afisa aliandika ‘Sonjo’ kwenye kitabu chake, badala ya kuandika hawa ni Batemi, na mazao ni sonjo. Kumbe, mpaka leo kumbukumbu hii ipo na nguvu, na watoto wanaendelea kucheka wanaposikia ‘sonjo’ imetoka wapi!

Your encouragement is valuable to us

Your stories help make websites like this possible.